Ijumaa , 11th Feb , 2022

Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 10 waliojipatia fedha za udanganyifu zaidi ya shilingi bilioni 2 baada ya kuchezea mfumo wa kampuni ya Selcom Paytech Limited, huku sehemu ya fedha hizo zikiokolewa kwani walizifukia kwenye mashamba.

Sehemu ya fedha zilizookolewa na Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 11, 2022, na Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi, na kusema wizi huo ulifanyika kwa njia ya mtandao katika maeneo mbalimbali ya Iringa, Dar es Salaam na Morogoro baada ya wakala Tyson Kasisi, kufanikiwa kuchezea mfumo na kisha kujitumia fedha pamoja na kuwatumia watu wengine kwa kushirikiana na genge lake la uhalifu.

Aidha Kamanda Bukumbi amesema kuwa mali ambazo ni mazalia ya uhalifu zimekamatwa na kuhifadhiwa ikiwa ni magari manne yenye thamani ya shilingi milioni 303,000,000 huku fedha zingine ambazo ni mazalia ya uhalifu huo kiasi cha shilingi milioni 121,215,783, zikizuiliwa katika moja ya benki za biashara mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa Kamanda Bukumbi amesema ushahidi uliokusanywa mpaka sasa umetosha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 10 kujibu tuhuma zinazowakabili kwa makosa ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.