Jumatano , 9th Jan , 2019

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Pius Msekwa amesema kwa mujibu wa sheria ya Bunge Spika, Job Ndugai ana mamlaka ya kumuuita kiongozi yeyote kwa mujibu wa sheria endapo atakiuka taratibu na sheria za kibunge.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) , Profesa Mussa Assadi , na Spika Job Ndugai

Spika Mstaafu Msekwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv juu ya sakata linaloendelea sasa juu ya kuitwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) , Profesa Mussa Assadi katika Kamati ya Maadili ya Bunge ili kujibu tuhuma juu ya kauli yake iliyodai kuwa Bunge ni dhaifu.

Msekwa amesema, "Spika anayo mamlaka ya kumuita mtu yeyote aje mbele ya Bunge ni kwa mujibu wa sheria ya Bunge na inampa sifa Spika na uwezo alioutumia, hata ningekuwa mimi ningemuita CAG, haiwezekani Mtanzania kaenda nje ya nchi akaanza kulaumu Bunge la Tanzania."

"Ni kosa kubwa sana anastahili kukemewa na mamlaka ya Bunge, hakuna tatizo ila CAG ndiye aliyeleta tatizo, hata kama alitoa maoni yake binafsi angeweza kutoa maoni yake hata akiwa ndani ya nchi", ameongeza Spika Mstaafu Msekwa.

Hivi karibuni akinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Profesa Ludovick Utouh alisema kutokana na utata wa suala hilo busara inapaswa kutumika ili kulimaliza.