Ijumaa , 4th Oct , 2024

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kusambaza umeme kwenye vitongoji 166 vilivyopo mkoa wa Morogoro baada ya kukamilisha usambazaji wa nishati hiyo kwenye vijiji 652 kati ya 669  ikiwa ni sawa na asilimia 97.5.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima

Mradi huo wenye gharama ya shilingi bilioni 17.9 unatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi 24 na utakapokamilika utanufaisha zaidi ya kaya 5,478.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha Mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya SINOTEC CO. LTD, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo pamoja na kuwapongeza REA kwa kusimamia vyema maono ya Mhe. Rais kuhakikisha wananchi wa vijijini nao wanapata maendeleo kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme.

"Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati, Mkoa wa uzalishaji na tumejipanga kuwa mkoa namba moja katika kilimo nchini na kuwepo kwa umeme maeneo ya vijijini kutasaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, umeme ndio nguzo namba moja katika kuongeza thamani mazao ya kilimo tuendelee kumpongeza na kumshkuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha zinazoenda kuwezesha zaidi ya vitongoji 166 vinapata umeme," amesema RC Malima.

Mhe. Malima pia ameendelea kuwasisitiza wananchi kutunza miundombinu ya umeme na kumtaka pia mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango vya ubora vinavyokubalika.

Awali akitoa taarifa ya upelekaji wa umeme Vijijini, Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Kati, Mhandisi Aneth Malingumu amesema kuwa kati ya vijiji 669 katika mkoa wa Morogoro, vijiji 652 ambavyo ni sawa na asilimia 97.5 vimefikiwa na nishati ya umeme na kuongeza kuwa vijiji 17 vilivyobaki viko kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji na kabla ya Oktoba 20 vitakuwa vimepata umeme.

Kwa upande wa vitongoji, Mhandisi Malingumu amesema kuwa mkoa wa Morogoro una jumla ya vitongoji 3,369 na katika hivyo, vitongoji 1,655 sawa na asilimia 49 tayari vimepatiwa umeme.