Jumamosi , 21st Jun , 2025

Mkutano wa siku mbili wa Jumuiya ya Ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu (OIC), unaofanyika katika muktadha wa mzozo unaoendelea kati ya Iran na Israel umefunguliwa leo Jumamosi (21.06.2025)

Kulingana na shirika la habari la Uturuki Anadolu, mamia ya washiriki wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.
Miongoni mwao ni mawaziri wapatao 43 na wawakilishi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi tayari amewasili Istanbul kushiriki mkutano huo, unaofanyika siku moja baada ya Araghchi kufanya mazungumzo mjini Geneva juu ya  suluhisho la kidiplomasia katika mzozo huo  na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka mataifa ya Ulaya, ikiwa ni pamoja na Johann Wadephul wa Ujerumani, Jean-Noël Barrot wa Ufaransa na David Lammy wa Uingereza.

Makabiliano kati ya Israel na Iran yameingia katika wiki ya pili huku mashambulizi ya kila upande yakiendelea licha ya kuwepo juhudi kadhaa za kidiplomasia ili kutuliza hali ya uhasama baina ya nchi hizo mbili.