
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Taarifa hiyo ameitoa hii leo Julai 24, 2020, na kusema kuwa hana maneno ya kutosha kuelezea kushtushwa kwake na taarifa za msiba huo na kwamba yeye pamoja na wanachama wa CHADEMA wanaungana na Watanzania kuombeleza msiba huo, na kutoa pole nyingi kwa mjane Mama Anna Mkapa.
"Familia nzima ya CHADEMA na familia yangu binafsi, tunaungana nawe, Mheshimiwa Rais na Familia nzima ya Hayati Mzee Benjamin William Mkapa, katika kuomboleza msiba huu mkubwa huku tukimshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha aliyomkirimu mja wake huyu kwa miaka yote na zaidi kwa utumishi wake kwa Taifa la Tanzania na Jamii ya Kimataifa" amesema Mh Mbowe.
Aidha Mbowe ameongeza kuwa, "Namtambua Mzee Mkapa kama mtu aliyekipenda sana Chama chake cha CCM, na aliyekuwa tayari kukilinda kwa nguvu za ziada hata pale alipotegemewa kwenda hatua moja zaidi kuonyesha kwa vitendo dhana na thamani ya Demokrasia ya kweli kwa Taifa letu, kipekee akiwa Rais aliyeko Madarakani au hata baadaye kama Rais Mstaafu".
Mbali na hayo Mbowe pia amekizungumzia kitabu cha Hayati Benjamin Mkapa, "Kama mwandishi mbobezi, kupitia kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’, Hayati Mhe Mkapa ameacha alama kubwa kwa kizazi cha sasa na vingi vijavyo na kutoa funzo kwa viongozi wengine kuelewa kuwa uongozi ni dhamana ambayo wanapaswa kuitumikia kwa unyeyekevu na tahadhari kubwa, wakiwa madarakani kwa manufaa ya wananchi na kuepuka kujutia baada ya kuachia nafasi hizo".