Jumapili , 15th Dec , 2019

Mkurugenzi Mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu hapa nchini (LHRC), Dkt Hellen Kijo Bisimba, amesema miongoni mwa mambo anayoyakumbuka wakati wa utumishi wake ni pamoja na lile tukio la mgomo wa madaktari lililotokea mwaka 2012.

Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu wa LHRC, Dkt Hellen Kijo Bisimba.

Hayo ameyabainisha wakati akifanyiwa mahojiano maalumu na East Africa Television, ambapo amesema kuwa wao waliamua kuwa upande wa madaktari katika kudai haki ya wagonjwa na si kwa maslahi ya mishahara kama ambavyo watu waliaminishwa.

"Sisi tulikuwa upande wa haki na unajua wale Madaktari hawakuibuka tu wakagoma, wale nao ni binadamu walikuwa na hoja na walikuwa washazipeleka Serikalini na wakapewa ahadi, walikuwa wanaumia sana wanapofika Hosptali wanashindwa kumsaidia mgonjwa ili hali wanao uwezo wa kutoa msaada, mfano walizungumzia suala la ukosefu wa cannula ambayo inauzwa 3000 tu" amesema Kijo Bisimba.

Aidha Dkt Kijo Bisimba ameongeza kuwa, "Sisi tulikuwa tunasisitiza Serikali iwasikilize madaktari, iwapatie vile vitu wanavyovihitaji na Serikali yenyewe ilikuwa imejikita kusema madaktari wanataka kuongezwa mishahara, lakini kikubwa haikuwa kuongezwa mishahara, walikuwa wanahitaji vifaa na kwa kukosa vifaa watu wengi wanafia mikononi mwao, kwahiyo ndugu waliofiwa wenyewe wanafahamu kabisa kwamba, kuna wakati wanaenda na mgonjwa hospitali wanaambiwa leo hatuwezi kumtibu kwa sababu hatuna mashine ya X-ray".