Jumanne , 16th Feb , 2016

Mgawanyo mbaya wa rasilimali nchini ndio chanzo cha tatizo la umaskini hasa maeneo ya vijijini na kwenye makundi ya watu wenye mahitaji maalumu hasa ya walemavu,wanawake,watoto na wazee.

Mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa kijinsia nchini TNGP Lilian Liundi

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa kijinsia nchini TNGP Lilian Liundi kwenye mdahalo wa kutoa tathmini yao ya siku 100 ya serikali ya awamu ya tano kwa mlengo wa kijinsia na kuitaka serikali itekeleze na kuzingatia usawa wa kijinsia ambao itakuwa ni rahisi katika utekelezaji wa majukumu kwa kuwafikia walengwa wa chini ambao ni wananchi bila ubaguzi.

Liundi amesema kwa zile pesa ambazo zimeokolewa kuwe na mfumo ambao utazifanya kweli pesa hizo ziende zikaboreshe huduma za jamii hasa zile ambazo zinawagusa watu wengi kama vile huduma za afya na elimu pamoja na utendaji ulioanza kujengewa mfumo endelevu.

Kwa upande wake mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es salaam UDSM kwa kitivo cha siasa na utawala Dr. Alexander Makulilo amesema serikali iangalie kwa umakini maswala ya urithi hasa kwa watoto wa kike na usimamiwaji wa elimu.