Alhamisi , 29th Jul , 2021

Mbunge wa jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi, amefanikisha ujenzi wa daraja la muda katika Mto Mngeta ambalo kwa muda mrefu limekuwa likihatarisha maisha ya wananchi wa Kata ya Mngeta, ujenzi wa daraja hilo la muda umegharimu kiasi cha shilingi milioni 31.

Daraja la muda lililojengwa na Mbunge wa Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi.

Februari mwaka huu ikiwa ni miezi mitatu tongu aanze kazi ya kuwatumikia wananchi wa Mlimba, Kunambi alifanya ziara jimboni kwake na kubaini changamoto ya kivuko kwenye Mto Mngeta, kwani wananchi wa eneo hilo kwa muda mrefu wamekuwa wakipata changamoto ya kivuko.

"Fabruari mwaka huu nilikuja hapa kujionea changamoto hii ya kivuko na nikawaahidi kwamba hakuna mwananchi mwingine ambaye ataliwa na Mamba mimi nikiwa Mbunge wenu, imani mliyonipa mimi na Rais wetu Samia Suluhu Hassan ndiyo ambayo imelipa leo ambapo sasa tumekamilisha ujenzi wa daraja hili la muda lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 31," amesema Mbunge Kunambi.

“Lengo langu kama mbunge wenu ni kuhakikisha tunapata daraja la kudumu ili kuondoa kero hii lakini kwa hatua hii ya kuweka kivuko cha muda ninaimani kuwa kutachochea maendeleo ya wananchi wetu na kuongeza usalama kwa watumiaji wanaopita hapa," ameongeza Kunambi