Jumatano , 7th Sep , 2016

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman Haikaeli Mbowe ameiomba serikali mjini Dodoma itoe upendeleo kwa shule zote ambazo wazazi wamejitahidi na kuanzisha mabweni kwa ajili ya kidato cha tano na sita ili yaweze kukamilika.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Haikaeli Mbowe

Mbowe ameyasema hayo katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, ambapo ameiomba serikali isaidie wazazi ambao wameonyesha nia ili shule hizo ziweze kufaidisha wengi hasa katika jimbo lake la Hai.

Akitolea maelezo suala hilo Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jaffo amesema kutokana na umuhimu wa elimu na namna ambavyo baadhi ya wazazi wamejitoa ni lazima serikali itafanya linalowezekana kuweza kuwaunga mkono.

“Tutaweka kipaumbele katika eneo hilo na ushauri wako ni mzuri kwetu na kweli kuna maeneo ambayo nimepita na kujionea na tunawapongeza wazazi wote wanaojenga mabweni ili wanafunzi wanaofaulu wasikose sehemu za kusomea na kulala” Amesema Jaffo.