Jumatatu , 26th Jun , 2023

Serikali imewatahadharisha wananchi mkoani Iringa kuacha kutembea usiku ili kuepukana na madhara ya kuvamiwa na Simba walioingia katika makazi ya watu, ambao mpaka sasa wameua ng’ombe 33,nguruwe 11,mbuzi 6 na kondoo watano.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega aliyetaka kujua nini mkakati wa serikali wa kuhakikisha wananchi wa Iringa wanaishi kwa uhuru kutokana na changamoto ya Uvamizi wa Simba.

"Niendelee kutoa elimu kupitia Bunge hili kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa Simba wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku lakini pia wenye mifugo wawashe mioto kuzunguka maeneo ya mifugo ili kuepusha Simba wasisogee katika maeneo yao," amesema Naibu Waziri Masanja

Kufuatia hatua hiyo Masanja amesema serikali tayari imeshapeleka helikopta inayozunguka usiku na mchana kuhakikisha Simba hao wanapatikana na kurudishwa katika maeneo yao ili kuhakikisha  maisha ya Watanzania yanalindwa kwa gharama yoyote

Kuhusu mikakati ya Serikali ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, Mhe. Masanja amesema serikali inatekeleza mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024 ambapo Wizara inatoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu, inajenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda (GPS collars) tembo; na kuanzisha timu maalum (Rapid response Teams).

Aidha, amesema Serikali imeshaweka mipango ya kujenga fensi ya umeme katika baadhi ya maeneo ili kupunguza athari ya wanyama wakali na waharibifu.