Jumatano , 15th Oct , 2025

Marekani imewataka wadau wote nchini Madagascar kutafuta suluhisho la amani linaloheshimu katiba baada ya kikosi maalumu cha jeshi CAPSAT kutwaa madaraka nchini humo.

Kikosi hicho kilitangaza kimeidhibiti nchi hiyo ya kisiwa cha bahari ya Hindi baada ya wabunge kupiga kura kumuondoa madarakani rais Andry Rajoelina.

Hatua hiyo inakuja kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kuipinga serikali ya Madagascar  yaliyochochewa na ghadhabu za wananchi kuhusiana na uhaba wa umeme na maji.

Kulingana na sheria ya Marekani, serikali ya Washington inatakiwa ikatishe msaada kwa nchi iliyoshuhudia mapinduzi ya kijeshi,  ingawa tayari utawala wa rais Donald Trump ulisitisha msaada wa Marekani kote ulimwenguni. 

Kwa mujibu wa data rasmi, Marekani iliipa Madagascar msaada kiasi dola milioni 32 katika mwaka wa fedha uliokamilika mwezi uliopita, kiwango kikubwa kikitengewa sekta ya afya.