Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Kichere leo amebainisha hayo wakati akizungumza na wanahabari na kusema kwamba Kanisa hilo limekuwa likitunza kiasi kikubwa cha fedha kwenda ndoo na ‘majaba’ kinyume na taratibu za utunzaji fedha.
Aidha taarifa hiyo kutoka Mamlaka ya Mapato imesema kwamba Kanisa halitengenezi hesabu za mapato na matumizi ya fedha kitu ambacho ni kinyume na katiba ya kanisa na sheria ya usimamizi wa fedha ambayo imepelekea matumizi mabaya ya fedha za waumini kama vile safari za nje ya nchi ambazo zimedhaminiwa na kanisa lakini wanaosafiri ni Askofu na familia yake.
Pamoja na hayo taarifa hiyo imedai kubaini kuwa Askofu Kakobe ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa zilizopo katika benki ya NBC zenye jumla ya kiasi cha Sh8.2bilioni, ambapo kiasi hicho cha fedha kimetokana na sadaka, zaka na changizo ambazo zinatolewa na waumini wa kanisa tajwa , hivyo kwa mujibu wa sheria hakitozwi kodi huku ikiongezwa kuwa Kanisa hilo lilikwepa kulipa kodi kiasi cha Sh20.8milioni.
Imeongezwa kuwa Kampuni inayomilikiwa na watoto wa Askofu Kakobe ilikwepa kulipa kodi ya Sh37.2 ambazo zimelipwa baada ya uchunguzi. Kwa ujumla kiasi kilicholipwa kutokana na uchunguzi ni Sh58.1milioni.
Hata hivyo Kamishna Kichere ameweka bayana kwamba Kakobe alimuandikia barua ya kumuomba radhi Rais John Magufuli kutokana na matamshi yake kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali .

