Jumanne , 8th Sep , 2015

Maonesho ya kibiashara ya wiki ya unywaji wa maziwa yanatarajiwa kufanyika mkoani Tanga kwa siku mbili kuanzia tarehe 18 mpaka tarehe 19 Mwezi huu katika viwanja vya Tangamano Jijini Tanga.

Dkt. Ruth Rioba Mwenyekiti wa Bodi ya maziwa taifa, akifafanua jambo juu ya kuleta maadhimisho ya wiki ya maziwa

Maonesho hayo yatashirikisha makampuni kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ambazo zitapata fursa ya kufanya biashara katika viwanja hivyo.

Akizungumza mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Maziwa mkoani Tanga Julius Show amesema makampuni zaidi ya 60 yanatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo yakiwemo makampuni ya utoaji wa pembejeo za mifugo pamoja na taasisi za utafiti na taasisi za mafunzo ya kilimo.

Lengo kuu la maonesho hayo ni kufanya mahusiano ya kibiashara kwa kuwakutanisha wadau wa maziwa na wadau wa makampuni mbalimbali ili kuwa na mtandao utakaoweza kutumika katika biashara katika siku za baadaye kwa kuwaletea pembejeo za kilimo.

Aidha Bw. Shoo amesema wafugaji watapata fursa ya kukutana na makampuni mbalimbali pamoja na wadau ili kuweza kupata huduma ya moja kwa moja na kuwaomba wakazi wa jiji la Tanga kujitokeza kwa wingi kushiriki.