Jumatatu , 2nd Jun , 2014

Mama mzazi wa Mbunge wa Kigoma kaskazini Zitto Kabwe, Bi. Shida Salumu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) na pia mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA Bi Shida Salum, anatarajiwa kuzikwa hii leo.

Marehemu Shida Salum ambaye ni mama mzazi wa mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe. Hii ni picha aliyopiga wakati wa enzi za uhai wake.

Marehemu amefariki jana katika hospitali ya Ami iliyopo Masaki Jijini Dar-es-salaam ambako alikuwa amelazwa baada ya kuugua kwa siku kadhaa.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Salum Kabwe ambaye ni kaka wa Zitto, alisema mama yao anatarajiwa kuzikwa leo saa saba mchana katika kijiji cha Mwanga kilichopo manispaa ya Ujiji Mkoani Kigoma.

Wakati huohuo, Mtoto Nasra Mohamedi ambaye alilazwa katika hospital ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam nchini Tanzania akitokea mkoani Morogoro ambako anadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na mama yake mkubwa kwa kumuweka ndani ya boksi tangu akiwa na umri wa miezi mitatu hadi kufikia miaka minne amefariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Akizungumzia kifo cha mtoto Nasra Momahedi, Afisa uhusiano wa hospital ya taifa ya Muhimbili Bw. Aminiel Eligaisha amesema mtoto Nasra amefariki dunia licha ya jitihada kubwa za madaktari walizozionesha katika kumtibu kwa lengo la kuokoa maisha yake.