Jumatano , 4th Oct , 2023

Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga, limesema tayari lina baadhi ya majina ya watu wanaojihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya mkoani humo ambapo limewataka wale wote wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo kujisalimisha mapema kabla hajatiwa nguvuni. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi, ametoa kauli hiyo wakati wa zoezi la matembezi maalumu waliyoyafanya ya kutembea zaidi ya kilomita 10 lengo likiwa ni kuimarisha amani. 

Kamanda Mchunguzi amesema jeshi hilo limeshaanza zoezi la kuwasaka wale wote wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo wakiwemo wauzaji wakubwa ambao wamekuwa ndio chanzo kikubwa cha kusambaa kwa dawa hizo.  

"Kwetu hapa kuna baadhi ambao ni watumiaji japo sio wengi sana lakini kwetu ni kama njia ya kwenda katika mikoa mingine, ukizingatia sisi tupo mpakani zoezi hilo limeanza na baadhi ya watu wanakamatwa na mpaka sasa tumeshawakamata watu wengi itakapofika muda nitawapeni taarifa ya watu hao, "amesisitiza Kamanda Mchunguzi

Aidha Kamanda Mchunguzi ameongeza kuwa, "Tunaendelea kuwasaka hasahasa wale wakubwa zaidi kwa kuwa tukipambana na hawa wakubwa wale wadogo itakuwa rahisi sana kwahiyo lengo letu ni kupambana na wale wakubwa zaidi ambao tayari majina yao tunayo, "