Ijumaa , 25th Mei , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa ufuta wasikimbilie kuuza zao hilo kwa wanunuzi wasio rasmi maarufu kwa jina la 'choma choma' bali wasubiri minada itangazwe mwezi ujao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua uwanja mpya wa michezo unaojengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Ninawasihi msikubali kuuza kwa akina 'choma choma' bali tumieni Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani, tumeona mfumo huu ulivyosaidia kwenye korosho,” amesema.

Kuna wawakilishi wa Kampuni ya Hyseas International Investment (T) Limited ya kutoka China ambao wamekuja hapa kuonana na uongozi wa Halmashauri. Wamesema watanunua ufuta wote uliolimwa Ruangwa na Nachingwea, ndiyo maana ninawasihi msubiri, msikimbiile kuuza ufuta kwa sasa,” Majaliwa.

Amesema kampuni hiyo imeahidi kuweka vituo vya ununuzi kwenye kata za Mandawa, Nanjaru, Nangurugai, Machang’anja hadi Mbangala ili wakulima wasihangaike kusafirisha ufuta wao. “Tunataka mwaka huu, wakulima wa ufuta nao wapate hela nzuri,” .