Jumamosi , 8th Jul , 2023

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Bi Tatu Isike kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya cha Mkunwa baada ya kubaini ujenzi umesimama kwa muda mrefu jambo linaloweza kusababisha kuharibika kwa vifaa vilivyonunuliwa bila kutumika.

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake mkoani Mtwara ambapo ameweka jiwe la msingi jengo la halmashauri ya wailaya ya Mtwara, ametembelea hospitali ya halmashauri ya wilaya ya mtwara ya Nanguruwe na mradi wa shule ya sekondari Dinecha halmashauri ya mji Nanyamba.

“Kwanza ujenzi ulisimama nimeuliza hilo sioni sababu, na hapa panaonekana pamefyekwa jana kwa sababu mimi nakuja leo, Nimemwambia Mkurugenzi kwa sababu yeye tu ndiye amekuja juzi  asimamie tabia hii Mkunwa asijitokeze” –Amesema Majaliwa.

Wananchi mkoani Mtwara wamejitokeza kwa wingi kumpokea Waziri mkuu na wameshukuru kwa ujio wake kwani ujio wake umekuwa fursa ya wao kusikilizwa kero zao huku wakiwa na matumaini makubwa ya kupata huduma bora za afya mara tu ujenzi wa kituo cha afya cha Mkuna utakapokamilika.