Jumatatu , 10th Sep , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, ameeleza kusikitishwa na Watanzania wanaoona aibu kuongea Kiswahili na kujilazimisha kuongea Kiingereza.

Rais Magufuli

Rais ameyasema hayo jana kwenye mkutano wake wa hadhara wilayani Meatu mkoani Simiyu na kutolea mfano Mwakilishi Mkazi wa Shirika la kimataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) Bi. Jacqueline Mahon ambaye amekuwa akitumia lugha ya Kiswahili.  

''Uzalendo wetu ni kulinda cha kwetu unaweza ukaona hapa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la kimataifa (UNFPA) Bi Jacqueline Mahon, anatoka Ulaya na amekipiga Kiswahili vizuri tu lakini unakuta Mswahili wa Tanzania ambaye anatakiwa kuitangaza lugha yetu anaogopa anataka azungumze Kiingereza'', alisema.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la kimataifa (UNFPA) Bi Jacqueline Mahon

Katika mkutano huo Bi. Jacqueline alieleza mikakati ya (UNFPA) katika kuhakikisha idadi ya watu nchini haipungui kwasababu ya changamoto za kiafya ndio maana shirika hilo limefanikisha ujenzi wa vituo vya afya mkoani Simiyu.

Rais Magufuli leo anakamilisha ziara yake katika mikoa ya Kanda ya ziwa ambayo ilianza Septemba 3, 2018 mkoani Mwanza kisha akapita Mara na leo anamalizia mkoani Simiyu ambapo ataweka jiwe la msingi katika ujenzi wa daraja la mto Sibiti pamoja na kuhutubia wananchi.