Jumanne , 25th Nov , 2014

Wataalamu wa tiba na Afya ya Mifugo Tanzania, wametakiwa kusimamia vizuri, sekta ya mifugo na mazao yake, kwa kuboresha machinjio ya nyama nchini, sanjari na kukagua mifugo inayochinjwa kila siku.

Wahudumu wa Machinjio wakashughulika na Uchinjaji wa Ng,ombe na Mbuzi.

Wataalamu wa tiba na Afya ya Mifugo Tanzania,wametakiwa kusimamia vizuri, sekta ya mifugo na mazao yake, kwa kuboresha machinjio ya nyama nchini, sanjari na kukagua mifugo inayochinjwa kila siku, kwani idadi kubwa ya mifugo inayochinjwa imeelezwa kutopimwa, jambo linalopunguza thamani ya nyama kwenye soko la kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Msajiri wa Baraza la Mavetenari nchini, Dokta Vedamu Msuruli, wakati akifungua mkutano wa tisa wa chama cha wataalamu wasaidizi wa tiba na afya ya mifugo Tanzania (TAVEPA), unaofanyika kwa siku tatu jijini hapa.

Dokta Msuruli ameeleza wataalamu wa mifugo nchini, wengi wao hawajitambui na kushindwa kuitumia taaluma yao ipasavyo, kwa kuboresha sekta ya mifugo, hasa suala la uchafu kwenye machinjio mbalimbali nchini, ambalo limekuwa sugu hatua mbayo inapelekea nyama inayopatikana kutokuwa na ubora unaohitajika.

Ameongeza kuwa pamoja na serikali kujitahidi kutoa ajira kwa wataalamu hao, pindi wanapo maliza masomo yao, lakini anashangazwa kuona wanashindwa kutekeleza majukumu yao na hivyo kufanya sekta hiyo ishindwe kuondoa changamoto zilizopo.

Aidha amewataka wataalamu wa mifugo kuwekeza katika sekta hiyo na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kusafirisha mazao ya mifugo nje ya nchi.