Alhamisi , 8th Sep , 2016

Serikali imeanza mazungumzo na benki ya China ili iyakopeshe mabenki nchini ili na wao wawakopesha wajasiriamali wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya viwanda ili kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba bungeni mjini Dodoma ambapo amesema serikali ya China imeanzisha mfuko kwa ajili ya kuwaweza wafanyabiashara Afrika hivyo serikali haina budi kutumia fursa hiyo katika kunyanyua uchumi wa nchi.

Dkt. Kolimba amesema kuwa mfuko huo ambao umeshatengewa dola bilioni tano tayari wizara hiyo imeshatisha kikao cha pamoja kati ya benki ya maendeleo ya china na mabenki ya Tanzania ili kupewa utaratibu wa kupata fedha za mfuko huo ili watanzania waanze kupata mitaji haraka iwezekanavyo.

Aidha Dkt. Kolimba ameongeza kuwa ubalozi wa Tanzania nchini unaendelea na jitihada za kuwashawishi wawekezaji kutoka China kuja kufanya ziara nchini hatua ambayo imeenza kuzaa matunda kwa kampuni ya China kuja kutengeneza kiwanda cha Nondo mkoani Pwani.

Amesema kuwa tayari wizara yake imeshawaleta wawekezaji wengine kutoka nchini China ambao watawekeza kwenye zao la tumbaku ambapo mpaka sasa kilichobakia ni makubaliano ya mwisho kati ya wizara ya kilimo na wawekezajo hao kutoka China.