Alhamisi , 22nd Jun , 2023

Wizara ya Elimu imesema kiwango cha elimu kinachotolewa nchini kimeimarika licha ya uwepo wa dosari ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi hali iliyofanya baadhi ya mataifa kuleta wanafunzi wao kuja kupata elimu nchini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Profesa James Mdoe

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Profesa James Mdoe, wakati akifungua mkutano wa 11 wa wanasayansi katika Chuo Kikuuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS),amesema elimu ya Tanzania imepiga hatua ikiwemo elimu ya vyuo ambapo kwa chuo cha Muhimbili kimekuwa moja ya vyuo vitano bora barani Afrika hali iliyofanya baadhi ya mataifa kuleta wanafunzi wake kuja kupata elimu.

Kuhusu utafiti Profesa Mdoe amewataka wanasayansi nchini kuendelea kutumia tafiti na kufanya tafiti zitakazoleta tija  kwa jamii huku akiahidi  serikali kuendelea kusaidia kada ya utafiti nchini kwa kutoa fedha pamoja na kusomesha wanafunzi kwenye kada hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS Apolynali Kamambwa, amesema mkutano huo  ni sehemu ya mikutano inayofanywa katika chuo hicho ambapo yamesaidia kukifanya chuo hicho kuimarika kielimu na hivyo kuleta matokeo katika kutatua changamoto katika sekta ya afya .