Jumatatu , 11th Aug , 2014

Wizara ya ujenzi nchini Tanzania imekanusha taarifa kuwa kivuko cha MV Kigamboni ambacho hivi sasa ni kibovu kuwa kimepelekwa Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya matengenezo.

Waziri wa ujenzi nchini Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara katika jiji la Dar es Salaam, waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuli amesema kivuko hicho kinakarabatiwa katika karakana ya jeshi la wanamaji Kigamboni na kwamba taarifa za kuwa kimepelekwa Mombasa Kenya hazina ukweli wowote.

Kwa mujibu wa waziri Magufuli, Tanzania hivi sasa ina uwezo wa kutosha wa kuvifanyia ukarabati vivuko vyake tofauti na inavyodhaniwa, na kutoa mfano jinsi serikali ilivyoweza kukitengeneza kivuko kipya cha MV Magogoni chenye uwezo wa kubeba Tani 500 na kwamba haiingii akilini serikali hiyo hiyo ishindwe kukifanyia ukarabati kivuko chenye uwezo wa kubeba tani 160.

Aidha, Waziri Magufuli amesema wizara yake itatumia fedha za Tanzania shilingi trilion Moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kadhaa ya barabara zikiwemo za juu pamoja na madaraja.

Barabara hizo kwa mujibu wa waziri Magufuli, ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na tatizo la msongamano wa magari lililokithiri jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mbinu mpya ya ujenzi wa barabara za juu katika baadhi ya makutano ya barabara itasaidia kukabiliana na tatizo la foleni.