Jumatatu , 8th Jan , 2024

Jeshi la polisi mkoani Geita linawashikilia Askari wanne wa Uhifadhi kwa tuhuma za mauaji ya kijana Semeni Locket, mkazi wa Kata ya Nyamigota Geita kwa kumpiga risasi ya mkono iliyopitiliza kifuani, baada ya kumkuta ndani ya hifadhi ya msitu wa Samina akichanja kuni kinyume na utaratibu.

Mwili wa kijana

#EastAfricaTV imeshiriki maziko ya kijana Semeni Hamis Locket ambapo vilio na majonzi vikiwa vimetanda miongoni mwa wanafamilia waliompoteza mpendwa wao,Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe akiwa ameambatana na watumishi wengine wa serikali wametoa pole kwa famia ya kijana huyo.

"Sijafurahishwa na sitofurahishwa na kitendo kilichofanywa na mtumishi mwenzetu wa umma ambaye alienda kujichukulia hatua za kisheria mikononi mwake kwahiyo hapa tunapozungumza watumishi wanne wa maliasili wanashikiliwa na jeshi la polisi lakini pia miongoni mwao kuna mwananchi mwingine pia ambaye alikuwa ni sehemu ya mwenzetu Semeni waliokuwa wameingia kwenye eneo hilo la hifadhi," amesema DC Geita

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Nyamigota amesema "Yule aliyefanya vile hakuagizwa na serikali afanye vile hata kama kijana wetu alikuwa ameingia kwenye hifadhi kimakosa lakini askari yule alitumia nguvu kubwa kwa kuwa tuna viongozi wetu hapa mkuu wa wilaya yupo hapa na taratibu nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi kupitia vyombo vya serikali vilivyopo hapa,".

Wanafamilia pamoja na wananchi wa kijiji cha Nyamigota wameiomba serikali kuwachukulia hatua askari waliousika na kifo cha kijana semeni ili iwefundisho kwa watumishi wengine wa maliasili wanajichukulia sheria mkononi.

Semeni Hamisi Locket ameacha mke mmoja na watoto wawili.