Jumatano , 16th Mar , 2016

Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali imebaini uwepo wa maamuzi mabovu pamoja na njama za kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma, yaliyokuwa yafanywe na Wakala wa Umeme na Ufundi Serikalini TEMESA.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali PAC, Aesh Hilary.

Maamuzi na matumizi hayo ni katika zabuni ya ukarabati wa kivuko cha abiria kilichokuwa kipelekwe Mombasa nchini Kenya kwa ajili kufanyiwa ukarabati lakini kikarudishwa njiani kutokana na hofu ya ugaidi.

Wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde, wamesema maamuzi ya kupeleka kivuko hicho nchini Kenya ambacho hata hivyo baadaye kilirudishwa mapema kikiwa maeneo ya Bagamoyo, yalifanywa pasipo kupata kibali cha serikali.

Akijibu maswali ya wajumbe wa kamati, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Manase Le-kujan, ametaja sababu ya kivuko hicho kurudishwa kikiwa njiani kuwa ni kutokana na taarifa za kiintelijensia kuonyesha kuwepo kwa tishio la kigaidi kutoka kwa kundi la Al-shaabab hasa eneo la kina kirefu cha bahari nchini Kenya ambako kivuko hicho kingepitia wakati kikielekea bandari ya Mombasa.

Majibu hayo yakamlazimu Mwenyekiti wa Kamati mhe. Aesh Hillary kuamuru kusitishwa mara moja kwa mpango wa malipo yaliyokuwa yafanywe kwa mzabuni aliyetaka kufanya ukarabati huo ambaye alifungua shauri mahakamani na serikali kutakiwa kumlipa zaidi ya shilingi milioni mia mbili.