Jumatatu , 13th Oct , 2014

Jukwaa la Katiba nchini Tanzania, limemesema limeshangazwa na hatua ya bunge maalum la katiba kuviondoa vipengele vinavyogusa mahitaji ya msingi ya Watanzania ikiwa ni pamoja na nafasi ya wananchi kuvua ubunge iwapo mbunge wao hawajabiki.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba nchini Tanzania, Deus Kibamba.

Akiongea leo jijini Dar es salaam,mara baada ya kuipitia katiba hiyo inayopendekezwa Mwenyekiti wa JUKATA, Bw. Deus Kibamba amesema katiba inayopendekezwa bado inatoa fursa kwa viongozi kujilimbikizia madaraka huku mihimili ya dola bado ikiwa haijitegemei.

Kwa mujibu wa Kibamba, Katiba inayopendekezwa haijaonesha namna ya kumaliza kero zinazowakabili wananchi hususani masuala muhimu kama usimamizi wa rasilimali za nchi pamoja na utawala bora.

Katika hatua nyingine, Kibamba amesema Jukwaa limebaini kuorodheshwa kwa jina la mbunge wa kuteuliwa Bi. Zakia Maghji, kuwa ni mjumbe kutoka Zanzibar wakati ameingia katika Bunge Maalumu la Katiba akiwa kama mjumbe kutoka Tanzania Bara.

Madai hayo ya Jukwaa la Katiba yamekuja siku moja baada ya Chama cha NCCR Mageuzi kulilalamikia Bunge Maalumu la Katiba kwa kuingiza jina la Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kutoka Zanzibar Bw. Haji Ambar Khamis kuwa ni mmoja wa waliounga mkono kwa kuipigia kura ya Ndiyo rasimu ya Katiba inayopendekezwa.