Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia mara baada ya kuendesha gari la Mwendo Kasi katika kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Haraka (BRT) mara baada ya kufungua rasmi Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam.
Amesema lengo ni kuondokana tatizo la mabasi hayo kutumia muda mwingi kukatiza katika eneo hilo.
Rais Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa awamu ya kwanza ya mradi wa miundombinu ya utoaji huduma kwa mradi huo wa BRT uliogharimu shilingi bilioni 403, ambapo ametaka kuharakishwa kwa mchakato wa kukamilisha kuanza kwa ujenzi wa barabara hizo za juu za kuchepuka.
Rais Magufuli amesema awamu ya pili ya mradi mabasi yaendayo kasi itahusisha barabara ya urefu wa kilometa 19.3 inayotoka barabara ya Kilwa katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Mbagala rangi tatu, pamoja na ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Makhtar Diop wa kwanza kulia wavivuta kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI George Simbachawene pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Akitaja awamu nyingine amesema kuwa itahusisha barabara ya Nyerere hadi Gongolamboto yenye jumla ya urefu wa Kilometa 33.6 mradi, awamu ya nne ni barabara yenye kilomita 25.9 ikihusisha barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Tegeta, yenye urefu wa Kilometa 22.8 awamu ya tano yenye urefu wa Kilometa 27.9 kwa awamu ya sita miradi yote hiyo itafadhiliwa na Benki ya Dunia.
Mhe. Rais Magufuli ameiomba Benki ya Dunia kuharakisha mchakato wa kutoa fedha za mkopo utakaowezesha kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Ubungo (Ubungo Interchange) ili kuongeza ufanisi wa mradi.
Mhe. Dkt. Magufuli amesema nia ya Serikali yake ni kuifanya Dar es Salaam kuwa Jiji la kisasa kwa kuhakikisha inakomesha tatizo la msongamano wa magari ambapo pamoja na kutekeleza mradi huo pia itajenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kati ya Dar es Salaam na Morogoro na kujenga barabara za haraka (Express Road) kati ya Dar es Salaam na Chalinze hivi karibuni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Makhtar Diop wakati Msanii Mrisho Mpoto alipokuwa akitumbuiza.
“Tunataka Dar es Salaam liwe Jiji la kisasa, ndugu zangu wa Dar es Salaam nataka mniamini hivyo, hivi karibuni tunapitia tenda na tutapata Mkandarasi wa kuanza kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo kuna jumla ya kilometa 200 na treni zitakazopita zitatumia mafuta na umeme”
“Lakini pia mchakato wa kujenga barabara ya haraka (Express Road) kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze yenye njia 6 na hatua zote zimekamilika na kilichobaki ni mazungumzo na wakandarasi kabla ya kuanza kujenga” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika, kuhakikisha mradi huo unaendeshwa kwa faida, miundombinu yake inatunzwa vizuri, wananchi wananufaika kama ilivyokusudiwa na pia ametoa siku 5 kwa Jiji la Dar es Salaam kufanya uamuzi juu ya matumizi ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 5.8 zilizotolewa na mbia anayemiliki asilimia 51 ya hisa za kampuni ya UDA-RT.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema wizara yake itatekeleza mikataba iliyowekwa na Banki ya Dunia ili kukamilisha miradi mingine ya maendeleo ikiwa ni pamoja na reli na umeme.