
Rais Magufuli
Amewataka Watanzania kutumia siku ya kesho Aprili 26, kuutafakari Muungano ulioasisiwa na viongozi wakuu Baba wa Taifa, hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na hayati Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la virusi vya Corona.
Katika kuadhimisha miaka 56 ya Muungano, Mhe. Rais Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3973, ambapo kati yao, wafungwa 3717 wamesamehewa vifungo vyao na wafungwa 256 waliokuwa wanakabiliwa na adhabu ya kunyongwa mpaka kufa wamebadilishiwa adhabu.
Mhe. Rais Magufuli amesema ana matumaini kuwa wafungwa hao wamejifunza na kujirekebisha ili waungane na jamii katika kulitumikia Taifa wakiwa raia wema wanaozingatia sheria.
Aidha Rais Magufuli amewakumbusha Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona, ikiwemo kujiepusha na mikusanyiko na safari zisizo za lazima.