
Tahadhari kubwa za joto kali zimewekwa katika miji mingi kuu ya Italia wakati joto linaongezeka Ulaya.
Joto linatarajiwa kuongezeka siku ya leo, huku miji 23 ikiwa katika hali ya tahadhari kuanzia Trieste kaskazini mashariki hadi Messina kusini magharibi.
Onyo hilo linamaanisha joto linaleta tishio kwa kila mtu, sio tu makundi yaliyo hatarini. Moto wa porini pia unaenea kote barani Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ugiriki na Alps ya Uswisi.Mamilioni ya watu katika eneo la kaskazini mwa dunia wanaathiriwa na joto kali.
Hali hiyo Inasababishwa na mfumo wa shinikizo la juu unaoleta hewa ya joto, ya kitropiki. Vilevile joto linatabiriwa kudumu hadi Jumatano katika sehemu kubwa ya kusini mwa Ulaya, kufuatia siku kadhaa za joto zaidi ya nyuzi joto 40.
Wimbi la joto, ambalo limeenea kote nchini Italia, limeelezewa na vyombo vya habari vya ndani kama wiki ya kuzimu. Wizara ya afya ya Italia imevitaka vyumba vya dharura kote nchini humo kuamsha kile kinachoitwa tahadhari za joto, na kutoa kundi tofauti la wahudumu wa afya kutibu watu wanaodhurikaa na dalili zinazosababishwa na joto.
Kumekuwa na ongezeko la asilimia 20 ya idadi ya wagonjwa wanaolazwa na dalili zinazohusiana na joto, kama vile upungufu wa maji mwilini, uchovu, kiharusi cha joto, na kuchanganyikiwa, kulingana na wizara ya afya.