Jumapili , 13th Jul , 2014

Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema haoni sababu ya msingi iliyopelekea Bunge Maalum la Katiba kuvurugika zaidi ya "Mapepo"na kuwataka watanzania kuwaombea wajumbe waliosusia bunge hilo

Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema haoni sababu ya msingi iliyopelekea Bunge Maalum la Katiba kuvurugika kwa kuwa yote yaliyokuwa yakifanyika yalifanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni walizojipangia wajumbe wa bunge hilo.

Rais ameyasema hayo leo katika sherehe za kilele cha miaka 75 ya kanisa la TAG zilizofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Katika hotuba yake ya takribani saa moja, Rais amesema kuwa “MAPEPO” ndiyo yaliyovuruga bunge hilo na kuwataka watanzania waungane na maaskofu wote kuwaombea wajumbe wake ili mapepo yawatoke, na hatimaye warudi bungeni kumalizia mchakato huo.

Rais amesema anashangaa kuona majadiliano ya sura ya Kwanza na ya Sita yalikuwa yakienda vizuri lakini ilipofika wakati wa kupiga kura, baadhi ya wajumbe wakasusa bila masharti na kusema kuwa hawatarudi.

“Hayo ni MAPEPO, watanzania wote tuungane na wachungaji na maaskofu kuwaombea wajumbe hao, ili mapepo hayo yawatoke” Amesema Rais Kikwete.

Aidha Rais amesema anaungana na maaskofu wa kanisa hilo kuwataka wajumbe waliosusia Bunge hilo wafikirie upya, na warudi bungeni kwa maslahi ya watanzania.

Amempongeza msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi kwa kuanza majadiliano na viongozi wakuu wa vyama vya siasa vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR ili kumaliza tofauti zao na kuendelea na mchakato.

Rais Kikwete pia amewaonya watu, taasisi, na makundi mbalimbali yanayotoa matamko mbalimbali kuhusiana na sakata hilo na kuwataka wakae kimya, wawaache viongozi wa vyama hivyo waendelee na majadiliano.

Katika hilo amesema “Watanzania tutulie tuwaache wazungumze, sio kila siku huyu kasema hili huyu lile, miluzi mingi inapoteza mbwa……"

“ Inaonekana kuna watu wana tenda ya kugombanisha watanzania, watuambie wanalipwa nini, ili serikali tuwalipe waache kazi hiyo”

Rais Kikwete alilazimika kutoa maelezo hayo baada ya Askofu Mkuu wa kanisa la TAG Dkt Barnabas Mtokambali kumuomba aingilie kati mchakato huo.