Rais Kikwete akiwa ziarani mkoani Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Agosti 20, 2014 ameanza ziara ya Mkoa wa Morogoro kwa kuzindua Mfumo wa Huduma za Afya za Masafa – telemedicine – katika Kituo cha Afya cha Mwaya, Wilaya ya Ulanga, ambako mtoto mchanga wa kike wa umri wa saa chache amepewa jina la Salma, mke wa Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye amewasili Kijiji cha Mwaya, kwa helikopta akitokea Dar es Salaam, kuanza ziara hiyo ya siku saba Mkoani Morogoro, ameanza kwa kuzindua Mradi Mkubwa wa Kusambaza Umeme Vijijini Morogoro kabla ya kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Mwaya.
Kwenye Kituo hicho cha afya, Rais Kikwete ameambiwa na Daktari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Godfrey Mtei kuwa mradi umethibisha uwezo mkubwa wa kuokoa maisha ya akinamama waja wazito wakati wa kujifungua, kutokana na wataalam kubadilisha ujuzi na utaalam kwa njia ya mtandao wa internet na simu wakati wa kuwazalisha akinamama.
Dkt. Mtei amesema kuwa tokea mwaka 2010 kiasi cha akinamama 13,674 wamejifungulia katika vituo vya afya vitatu vya Mwaya, Mtimbira na Mlimba ambavyo viko katika Mfumo huo katika Mkoa wa Morogoro na kati ya hao 1,360 wamejifungua kwa upasuaji na vimetokea vifo tisa tu katika kipindi hicho chote.
Mfumo huo unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika Lisilokuwa la Kiserikali la World Lung Foundation ambalo linafadhiliwa, miongoni mwa taasisi nyingine, na Bloomberg Philanthropies, unatekelezwa katika Mikoa ya Pwani, Morogoro na Kigoma.
Miongoni mwa mambo mengine, World Lung Foundation linagharimia vifaa kama simu, kompyuta mpakato (laptops), moderms, linatoa mafunzo kwa watumishi wawili wawili kutoka kila moja ya vituo vya afya ambako Mfumo huo unaendeshwa na kutoa gharama ya vituo kuunganishwa kwenye mtandao.
Aidha, chini ya Mpango wa Kuboresha Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto, Shirika hilo pia linajenga vyumba vya upasuaji ikiwa ni pamoja na kutoa tiba stahiki, wadi za wazazi, uboreshaji wa mifumo ya maji na umeme kwa kuweka jenereta na sola, kujenga nyumba za watumishi na kutoa mafunzo mahsusi kwa watumishi wapatao 106.
Mara baada ya kuzindua Mfumo huo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete amemtembelea wodini mtoto wa kike ambaye amezaliwa leo hii chini ya Mfumo huo. Mama yake mtoto huyo ameamua kumpa mtoto huyo jina la Salma (la Mama Kikwete) mara baada ya Mama Salma kumbeba na kumfurahia mtoto huyo.
Kwenye makao makuu ya Wilaya ya Ulanga ya Mahenge, Rais Kikwete amezindua Hosteli ya wasichana katika Shule ya Sekondari ya Nawenge na pia kupokea madawati 100 kwa ajili ya shule ya msingi ya Epanko ambayo yametolewa na Kampuni ya Kibaran Resources ya Australia ambayo inafanya maandalizi ya uchumbaji wa madini ya uno – graphite – katika wilaya hiyo. Shule ya Sekondari ya Nawenge ina wanafunzi 475 na walimu 26. Aidha, Rais Kikwete amezindua mradi wa maji wa mjini Mahenge ambao umegharimiwa na Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 433.7. Mradi huo umejengwa kutokana na ahadi ya Rais Kikwete ya mwaka 2008 wakati alipotembelea Wilaya ya Ulanga.
Rais Kikwete pia amesimama Kijiji cha Lupiro ambako amezindua maghala ya kuhifadhi mchele baada ya kuwa umepukuchuliwa kutoka kwenye mpunga na kuhutubia mkutano wa hadhara ambako wananchi wametoa kilio chao kutokana na ukosefu la soko la uhakika la mchele.
Baada ya Lupiro, Rais Kikwete ameingia katika Wilaya ya Kilombero ambako ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero ambalo ujenzi wake umekuwa unazungumzwa na kupangwa kutokea mwaka wa fedha wa 1967-1968.
Rais Kikwete leo, Alhamisi, Agosti 21, 2014 anaendelea na ziara yake katika Mkoa huo wa Morogoro kwa kutembelea Wilaya ya Morogoro.