Jumatatu , 21st Oct , 2024

Idadi ya Watanzania waliojitokeza kujiandikisha imeongezeka kwa 8%, kwa mwaka 2024 ambapo wamejiandikisha watu milioni 31,282,331 Sawa na 94.82% ukilinganisha na uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,  Mohamed Mchengerwa  anasema kwa mwaka huu idadi hiyo imeongezeka kutokana na hamasa iliyotolewa kwa wingi ya umuhimu wa wananchi kujiandikisha.
"Watanzania milioni 31,282,331 wamejitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la makazi nchi nzima ikiwa ni Sawa na 94.83%, ya lengo la watu walio kwenye umri wa kujiandikisha ambao ni milioni 32,987,576 ambapo wanaume ni milioni 15,236,772 Sawa na 48.71% huku wanawake wakiwa milioni 16,045,559 Sawa na 51.29%", MOHAMED MCHENGERWA  --Waziri wa  TAMISEMI
Aidha Waziri Mchengerwa anasema Mkoa wa Pwani umeongoza kwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza kujiandikisha.
"Wananchi wa Mkoa wa Pwani wameongoza kwa kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mkazi ambapo watu zaidi ya 100% wamejitokeza huku mkoa wa Rukwa ukishika mkia ambapo wamejitokeza kwa 64.58%", MOHAMED MCHENGERWA  -Waziri wa  TAMISEMI.
Wananchi wametakiwa kuhakiki mjajina yao kwenye vituo walivyojiandikishia ili kufanya marekebisho endapo kuna kitu kimekosewa.
"Orodha ya wapiga kura kwenye kila kituo imeanza kubandikwa kuanzia leo ambapo wananchi wanaombwa kufika kwenye vituo walivyojiandikisha ili kuhakiki taarifa zao Kama kuna mahali zilikiwa zimekosewa na zoezi hilo litaenda kwa siku saba kuanzia leo Oktoba 21-27, 2024", MOHAMED MCHENGERWA  -Waziri wa  TAMISEMI.
Nao wananchi wanaelezea walivyojiandaa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Mimi nimejiandikisha kwa sababu najua sana umuhimu wa kupiga kura na ikifika tarehe 27, nitaenda kuchagua viongozi watakaonifaa", BAKARI SALUM-Mkazi wa Dar es Salaam.
"Nashauri wananchi wenzangu waweze kutumia fursa hii kuweza kupata viongozi wawatakao kuliko kuacha kupiga kura na baadae kuanza kulaumu", SHAMSI AKIDA-Mkazi wa Dar es Salaam.
"Niko tayari kupiga kura lakini naomba wananchi watuamini vijana wengi hatupewi nafasi kwa sababu hawatuamini wakati sisi tunaweza kuongoza vizuri jamii yetu", BAKARI HAMISI-Mkazi wa Dar es Salaam.