Jumanne , 15th Nov , 2016

Waziri wa Maliasili na utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amesema Tanzania haiko tayari kuuza magogo nje ya nchi na badala yake shughuli za kuvuna magogo hayo zitafanyika hapa nchini ili kuchochea uanzishwaji wa viwanda na ajira kwa wananchi wake.

Waziri wa Maliasili na Utalii (Kulia)

 

Akiongea na East Africa Radio mara baada ya kufungua mkutano wa wawekezaji wa misitu ya kupandwa ulioandaliwa na tasisi ya Uongozi Institute kwa kushirikiana na serikali ya Finland, leo jijini Dar es salaam. Mhe Maghembe amesema ni lazima uchakataji wa magogo ufanyike nchini ili kuliongezea taifa kipato.

Aidha, Mhe. Maghembe amewataka watanzania kujiingiza katika kilimo cha misitu ya kupandwa ili waweze kujikwamua kiuchumi na kumuongezea kipato kwani serikali itatoa fedha kwa mtu atakaye panda miti ambayo mbali na kipato pia husaidia katika kunyonya hewa ukaa.

“Mpango uliopo sasa ni kuakikisha kuwa kila mtu anafaidika na mti kuanzia atua ya awali hadi pale wakati wa kuvuna kwani mtu atalipwa fedha kwa namna gani miti yake inavyokuwa na kunyonya hewa ya ukaa inayodhalishwa viwandani hivyo hakuna mtu atakaye acha kupanda miti” Amesema Maghembe.

Amesema, Serikali ya Finlande itaisaidia serikali katika kuhakikisha inapima misitu yake kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwani bado Tanzania inatumia Teknolojia ya zamani ambayo aitenganishi magogo na miti lakini baada ya ushirikiano huo Tanzania itaweza kupima misitu kwakutumia ndege.

Amesema kuwa kwa mujibu wa ripoti iliyotoka mwaka 2014 inasema kuwa Tanzania imeweza kutunza jumla ya ekari 17 Milioni ambazo ni sawa na asilimia 35% ya ardhi yote ambayo ipo hapa nchini huku asilimia 85% ya malighafi inayosambazwa katika viwanda mbalimbali nchini inatotokana na misitu.