
Waziri Ummy Mwalimu
Akipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa tume hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama Dkt. Charles Majige Waziri Ummy amesema kuwa Bi. Asma Juma(29) hakuwa na watoto mapacha kama ilivyodaiwa na mlalamikaji huyo kutokana na kipimo cha Utra sound kukosea katika uchukuaji picha ya mtoto akiwa tumboni.
“Nimepokea taarifa kutoka kwa tume huru niliyoiunda hivi karibuni na imethibitisha kuwa Bi. Asma Juma hakuwa na watoto mapacha ila uchukuaji mbaya wa picha ya mtoto aliyekuwa tumboni uliofanywa katika zahanati ya Huruma ukatoa matokeo hayo” alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa wanafamilia ya Bi. Asma wanatakiwa kumfariji ndugu yao na sio kumkumbushia jambo hili mara kwa mara kwani litamharibu kisaikolojia na kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa mtoto kama mama mzazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Charles Majige amesema kuwa Bi. Asma aliamini hivyo kwa sababu Hospitali ya temeke hawakumchukua vipimo vya picha bali walitumia taarifa ya vipimo vya awali .
Aidha Dkt. Majige Amesema kuwa tume hiyo imebaini kuwa Bi. Asma hakuibiwa mtoto na alikua hana mapacha kwa sababu uzito wake ulikua sio wa kubeba watoto wawili na katika chumba cha upasuaji kulikua na wataalamu 6 kutoka vitengo mbalimbali.
Kwa upande wake mwakilishi wa Familia ya Bi. Asma Juma, Jordan Jaddah amesema kuwa anaishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya kufatilia jambo hilo kwa ukaribu na kupata ukweli wa malalamiko yao na wameikubali taarifa hiyo .
“Tunaipongeza tume hiyo chini ya Wizara ya Afya na tunashukuru kwa msaada wao mwanzo mpaka mwisho na kutupatia majibu ya kuridhisha nasi tutakuwa bega kwa bega katika kumfariji ndugu yetu kwa jambo hili lilitokea” alisema Bw. Jaddah.