Jumatatu , 22nd Nov , 2021

Serikali ya Kenya inapanga kutambulisha muongozo mpya wa kukabiliana na Uviko-19 Desemba 21 utakaozuia raia wake ambao hawajachanja kupata huduma kwenye majengo ya serikali.

Waziri wa Afya Kenya Mutahi Kagwe

Muongozo huo pia unazuia watu wasiochoma chanjo ya Uviko-19 kusafiri kipindi hiki cha Krismasi pamoja na kudhibiti unywaji wa pombe.

Waziri wa Afya Kenya Mutahi Kagwe amesema watu wasiochoma chanjo ya corona watazuiwa kutumia usafiri wa umma, usafiri wa anga wa ndani pamoja na wa reli.

Wananchi wa Kenya watalazimia kuthibitisha kuwa wamechoma chanjo ya Uviko-19 ili kuingia kwenye ofisi za umma kwa huduma za elimu, uhamiaji, kodi pamoja na huduma nyingine.

Kuanzia jumanne wiki hii vijana wa Kenya wenye umri wa kuanzia miaka 15 wataanza kupatiwa chanjo ya Uviko-19 aina ya Pfizer.

Hadi sasa ni asilimia 10 tu ya wananchi wa Kenya wameshapata chanjo ya Uviko-19, ambapo serikali inalenga kuwachoma chanjo watu milioni 10 ifikapo mwishoni mwa Desemba mwaka huu.