Alhamisi , 19th Sep , 2024

Wafanyabiashara waofanya shughuli zao Mtaa wa Ally Maua A, Kijitonyama wameiomba Serikali iwasaidie kupunguza gharama za mabango kwani zimekuwa kubwa ukilinganisha na mzunguko wa biashara zao.

Moja ya bango linalotakiwa kulipiwa

EATV ikafika kwenye maduka hayo na kushuhudia aina za mabango na kiasi ambacho wametozwa.
“Mimi hapa kwangu nilikuwa nimeandika hapa ukutani nikaambiwa nilipe 700,000/=, kwa mwaka biashara yangu ndogo ya kuuza CD na vitu vidogo vidogo kweli 700,000/= nitawezaje kulipa hayo yote”, alisema Jerome Shao-Mfanyabiashara.

“Sisi wafanyabiashara wadogo wadogo tulikuwa tunaomba Serikali ituondolee hii kodi kwa sababu biashara zetu bado ni changa na kipato chetu kidogo sana, utakuta mtu huna hata msingi wa milioni moja hapo hapo TRA, wanapita unatakiwa utoe mapato TRA, unatakiwa leseni sasa hivi tena mabango”, alisema  Angel Mbando-Mfanyabiashara.

“Sio kama hatupendi kulipa kodi hapana tunapenda kwa sababu sisi ni watanzania na maendeleo yetu tutayaleta sisi wenyewe lakini wangeangalia upya hii sheria ya kodi ya mabango inatuumiza sana bei ni kubwa mno na mabango tuliyokuwa tunajua yanalipiwa ni ya barabara kubwa sio mpaka pembeni”, alisema Baraka Kistosi-Mfanyabiashara.

“Kama Hali itaendelea hivi sisi tupo tayari kufuta haya mabango kwa maana Mimi natakiwa kulipa 315,700/=, kwa muda wa mwaka kiukweli na wametupa muda mfupi wa kulipa tungeomba watupunguzie gharama”, alisema  Ziada Mbegu-Mfanyabiashara.

EATV haikuishia hapo ikamtafuta Meneja wa chanzo cha Mabango kutoka Manispaa ya Kinondoni nae anatoa ufafanuzi kuhusu chanzo hicho cha mapato.
“Chanzo hiki kilikuwa TRA, kikarudishwa kwetu manispaa na kipo kwa Mujibu wa Sheria na kinalipwa kutokana na ukubwa na aina ya Bango lako niwatoe wasiwasi wananchi ambao wanahisi wanatapeliwa kwa maana chanzo hiki kinatambulika na sisi Kinondoni tunakiendesha, mabango yote ya biashara yanatakiwa kulipiwa ambapo square fit moja kwa bango linalowaka taa ni shilingi 10,000/=, kwa mwaka na bango ambalo haliwaki taa ni shilingi 7,000/= na kuna magari ambayo yapo branded kwa square fit moja ni shilingi 4,000/=“, alisema Jumanne Manji-Meneja Chanzo cha Mabango Kinondoni.

Nae Muhasibu wa Chanzo cha Mabango anasema wametakiwa kukusanya mapato ya shilingi bilioni 3 kwa mwaka mzima kupitia chanzo hicho.
“Chanzo cha mabango kipo kwa Mujibu wa sheria na kimeletwa mwaka huu wa fedha kutoka TRA kuja Halmashauri na tumeelekezwa kukusanya shilingi bilioni 3 kwa mwaka”, alisema Edson Masunga-Mhasibu chanzo cha mabango.