Ijumaa , 9th Mei , 2025

Hatimaye dunia imeshughudia kukamilika kwa uchaguzi uliompata Papa mpya ambaye atakuwa kiongozi wa 267 wa kanisa katoliki duniani

Kardinali Robert Prevost ametangazwa jana kuwa kiongozi ajaye wa Kanisa Katoliki. Yeye ndiye Papa wa kwanza kutoka Marekani na kuchukua jina la papa Leo XIV.

Kanisa Katoliki limempata Kiongozi wake mpya, Papa Leo wa 14 atakayewaongoza takriban waumini bilioni 1.4 kote ulimwenguni. Kiongozi huyo amepatikana Alhamisi jioni baada ya uchaguzi uliofanywa na makadinali wapatao 133 kutoka mataifa 70.

Papa Leo XIV, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Francis Prevost, alizaliwa huko Chicago Septemba 14, 1955.
Prevost alisoma katika Umoja wa Kitheolojia wa Kikatoliki wa Chicago, akitunukiwa diploma ya theolojia.
Akiwa na umri wa miaka 27, alikwenda Roma kusomea sheria za kanuni katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas (Angelicum). 

Mafunzo yake ya kidini yalimfikisha Peru kama mmishionari, na baadaye akafanikiwa kupata nyadhifa mbalimbali nchini Marekani na Peru.

Prevost aliongoza dayosisi ya Chiclayo huko Peru na alikuwa makamu wa pili wa rais wa mkutano wa maaskofu wa Peru.  

Papa Francis alifahamiana naye katika nchi hiyo ya Amerika Kusini na mwaka 2023 akamteua kuwa mkuu wa Baraza la Maaskofu, na kumfanya kuwa kardinali.

Baraza la Maaskofu ni idara ya wahudumu wa  Kanisa Katoliki. Katika jukumu hilo, amehusika na uteuzi wa maaskofu duniani kote kwa miaka miwili iliyopita. 

Wakati huo huo, Prevost alikuwa rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini.

Katika maneno yake ya kwanza kama Papa, Leo XIV alizungumza kwa upendo kuhusu mtangulizi wake Francis alisema Bado dunia ina majonzi na huzuni kuhusu kifo cha Papa Francis na kuitaka dunia kuendelea kuungana kumuombea apumzike kwa amani

Aliwaambia umati uliokuwa ukisikiliza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwamba alikuwa mwanachama wa Shirika la Augustino. 

Alikuwa na umri wa miaka 30 alipohamia Peru kama sehemu ya misheni ya Augustino
Francis alimteua kuwa Askofu wa Chiclayo nchini Peru mwaka mmoja baada ya kuwa Papa.
Anawajua vizuri Makadinali kote ulimwenguni kwa sababu ya nafasi yake muhimu kama mkuu wa Baraza la Maaskofu.

Kwa kuwa asilimia 80 ya makadinali walioshiriki mkutano mkuu waliteuliwa na Francis, haishangazi sana kwamba mtu kama Prevost alichaguliwa.

Ataonekana kama mtu aliyeunga mkono kuendelea kwa mageuzi ya Francis katika Kanisa Katoliki.
Ingawa ni Mmarekani, na atakuwa anafahamu kikamilifu mgawanyiko ndani ya Kanisa Katoliki, historia yake ya Amerika ya Kusini pia inawakilisha mwendelezo baada ya Papa aliyetoka Argentina.

Ingawa wakati wake kama askofu mkuu nchini Peru hakuepuka kashfa za unyanyasaji wa kijinsia ambazo zimegubika Kanisa, jimbo lake lilikanusha vikali kwamba alihusika na jaribio lolote la kuficha ukweli.

Kabla ya mkutano mkuu, msemaji wa Vatican Matteo Bruni alisema kuwa wakati wa mikutano ya Baraza la Makadinali katika siku zilizotangulia mkutano mkuu walisisitiza umuhimu wa kuwa na Papa mwenye roho ya kinabii inayoweza kuliongoza Kanisa ambalo halijifungi ndani bali linajua jinsi ya kwenda nje na kuleta mwanga kwa ulimwengu uliojaa kukata tamaa