Jumapili , 17th Jan , 2016

Ili kutekeleza agizo la serikali la kutoa elimu bure nchini Mkoa wa Dodoma umepokea zaidi ya Sh. 584 milion kwa ajili ya Elimu bure kwa shule za Sekondari na Msingi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Chiku Gallawa

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Chiku Gallawa kwenye kikao cha kazi cha watendaji wa sekta ya elimu ngazi ya halmashauri na Mkoa.

Gallawa amesema Mkoa huo umepokea sh. 244,089,000 kwa ajili ya shule za Msingi huku ruzuku ya uendeshaji ikiwa ni sh. 214,264,000 na sh.29,825,000 kwa ajili ya chakula.

Amesema pia Mkoa huo umepokea sh. 340,235,000 kwa ajili ya shule za Sekondari ikiwa ni kwa ajili ya chakula huku sh. 143,116,000 zikiwa ni kwa ajili ya fidia ya ada ya bweni.

Amesema pia wamepokea sh. 85,755,000 kwa ajili ya fidia za shule ya kutwa na sh. 88,888,000 kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji, hivyo kupokea jumla ya sh.584,324,000 kwa ajili ya shule za Msingi na Sekondari.

Mkuu huyo amesema Mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba pamoja na kidato cha nne hivyo kuwataka wanaohusika kuiondoa aibu hiyo.

Amesema kuwa katika matokeo ya darasa la saba mkoa huo ulishika nafasi ya 24 kati ya mikoa 25 na katika matokeo ya kidato cha nne ulishika nafasi ya 19 kati ya Mikoa 25,hizi ni nafasi mbaya hazikubaliki huu ni mkoa ambapo makao makuu ya Serikali na bunge tuoneane aibu.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda akitoa mada iliyohusu wajibu wa Watendaji kwa mwaka 2016 katika mkutano huo amesema,watendaji wa elimu wanatakiwa kufikiri, kupanga na kutekeleza ili kuinua taaluma katika mkoa wa Dodoma.

Kaponda amewataka watendaji hao kusimamia utekelezaji wa elimu, bure na kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayekiuka maagizo hayo.