Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akihutubia waumini wa dini ya kiislamu mkoa wa Mara katika ukumbi wa chuo kikuu huria mjini Musoma katika baraza la Eid El Hajj sherehe ambazo kitaifa zimefanyika mjini Musoma.
Amesema amani kwa taifa lolote lile ni sharti la kwanza katika mchakato mzima wa kuharakisha maendeleo ya wananchi na kwamba viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kujenga maadili mema kwa taifa hatua ambayo inawezesha kupunguzia mzigo serikali katika kutumia fedha nyingi kwa kujenga vituo vya polisi,magereza pamoja na vifaa kwa ajili ya kulinda amani.
Kwa sababu hiyo kiongozi huyo ambaye awali alihudhuria ibada ya sikukuu ya Idd amewataka watanzania kulinda umoja na mshikamano wa taifa na kwamba tofauti za dini, itikadi za kisiasa, rangi na makabila kamwe zisitumike kuwagawa wananchi kwa kutambua wote ni wamoja kwa kuzingatia maslahi ya taifa letu.
Kuuhusu uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu, makamu huyo wa Rais amewaomba viongozi wa dini nchini kuhamasisha waumini wao kujitokeza kupiga kura katika kuchagua viongozi wanaowataka bila vishawishi katika kutekeleza haki yao ya kikatiba.