Alhamisi , 6th Mar , 2025

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ametoa rai juu ya umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana na kuibua wagunduzi wake ili kuzalisha teknolojia yake badala ya kuendelea kuwa tegemezi.

Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo Machi 06, 2025 wakati akihutubia Mkutano wa 16 wa Mtandao wa Kamati za Bunge za Afya (NEAPACOH) unaofanyika jijini Dar es Salaam, ukiwa na kaulimbiu: "Kuweka upya nafasi ya wabunge katika utekelezaji wa ajenda ya ICPD isiyokamilika na kufanikisha Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).

Dkt. Mollel amesema Afrika ina rasilimali nyingi na vipaji vya kutosha kuunda suluhisho bunifu, hasa katika sekta ya afya, ambavyo vinaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi. 

"Niwashauri tuwe na programu za ubunifu ili kujitegemea kiteknolojia na kupunguza utegemezi wa bidhaa na huduma kutoka nje," Amesema Dkt. Mollel.

Aidha Dkt. Mollel, amesema kuwa uimarishaji wa Huduma ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage - UHC) utakuwa kichocheo muhimu cha kuboresha maisha ya wananchi katika Ukanda wa Afrika, kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za afya, ikiwemo matibabu ya VVU (ARVs) na kutokomeza kifua kikuu (TB) kwani lengo la UHC si tu kuwa na afya ya kuishi, bali kuwa na afya bora ya mwili na akili, ili wananchi waweze kufikiri vyema na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.

"Tunapozungumzia UHC, tunazungumzia zaidi ya matibabu ya magonjwa. Tunazungumzia kuboresha maisha ya watu, kuimarisha afya ya akili, na kuwezesha jamii zetu kuwa na nguvu za kiakili na kimwili kushiriki kikamilifu ujenzi w Afrika yenye ustawi," amesema Dkt. Mollel.

Mkutano huo umekutanisha wajumbe kutoka nchi za Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mifumo ya afya na maendeleo ya watu katika bara hilo.