Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro
Agizo hilo limetolewa leo Juni 28, 2024, na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bw. Said Kitinga wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi wa LTIP katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Amesema, kila kiongozi katika eneo lake atoe elimu sahihi kwa wananchi juu ya utekelezaji wa mradi huo ili utekelezwe kwa ufanisi na kutimiza lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa watanzania.
"Katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga takribani viwanja 40,474 vitatambuliwa, vitapangwa, vitapimwa na kumilikishwa kwa wananchi katika maeneo yatakayofikiwa na mradi pamoja na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi, kutoa elimu ya masuala ya ardhi pamoja na kutoa hamasa juu ya usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi," amesema Mtatiro
Ameongeza kuwa, utekelezaji mradi huo utahusisha utambuzi wa kila kipande cha ardhi, upangaji wa maeneo yote yaliyotambuliwa kwa kuandaa michoro ya mipangomiji, upimaji wa viwanja vilivyopangwa kwa kuweka alama za upimaji na kuandaa ramani za upimaji na wananchi kumilikishwa maeneo yao kwa kupewa hatimiliki.