Ijumaa , 9th Feb , 2024

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Bi. Judith Nguli amezuia leseni ya uvunaji miti aliyotaka kupewa mfanyabiashara Ahazi Mwilongo na uongozi wa Kijiji cha Bungoma kwa kushirikiana na Kata ya Mkindo baada ya mfanyabiashara huyo kuanza kuvuna miti iliyopo kwenye chanzo cha maji cha Mto Mkindo.

Mbali na mfanyabiashara huyo kuvuna miti iliyopo kwenye chanzo  hicho cha maji cha mto Mkindo inaelezwa pia alianza kufanya kazi hiyo kabla ya kukamilika kwa mchakato wa kibali chake kwa mujibu wa maelezo ya Sipendeki Lihundi ambaye ni mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkindo. 

"Sitakaa kimya pale ninapoona serikali yangu inafanya vitu vya tofauti, tarehe 10 jioni nilipata simu, kuna watu wanalima huko juu, mzee ilani ya chama chako inasimamia vitu gani? nikamwambia inasimamia vitu vyote, akasema huku juu miti inaisha" amesema mwenyekiti wa CCM, Kata ya Mkindo Sipendeki Lihundi

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero alilazimika kufika katika chanzo hicho cha maji ambapo ameshuhudia uharibifu wa mazingira uliofanyika katika eneo hilo la mto na kutoa maagizo baada ya kusikiliza uongozi wa kata, kijiji pamoja na mhifadhi wa wilaya kutoka TFS.

"Kweli kunamfanyabiashara amekuja,lakini bado tunaendelea na taratibu,ilikuwa tarehe 30 na yeye mwenyekiti alipokuja hakuniambia kama wamemkuta mtu na mali zake huko msituni" 

"Kwahiyo mimi nitumie nafasi hii kwa kuzuia leseni ya huyu bwana mpaka pale tutakapojiridhisha baada ya kufanya uchunguzi wa kina,lakini pia hili jambo linasintofahamu hivyo tuwape takukuru waliachunge na kuja na majibu" amesema mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli.