Jumatano , 21st Aug , 2019

Idadi ya watu waishio mijini nchini Tanzania inatarajiwa kufikia milioni 45 ifikapo mwaka 2030, na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 6 kwa ukuaji wa miji ulimwenguni,  huku Jiji la Dar es salaam, likikadiriwa kuwa na watu milioni 10 kabla ya mwaka 2035.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo

Utafiti huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dkt Tausi Kida leo Agosti 21,  wakati wa uzinduzi wa Utafiti huo na kuitaka Serikali kuwa na mipango mizuri ya miji.

''Miji mingi ya Tanzania inakua, wabobezi wa masuala ya watu na makazi mnaelewa kwamba changamoto inaweza kujitokeza pale Jiji linapopata hadhi na kuwa Jiji kubwa kwa kuangalia kasi hii ya ukuaji wa miji hapa nchini ni muhimu kwetu kama nchi kuwa na mipango mizuri ya miji''.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo,  ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuja na utafiti huo, na kusema kwamba licha ya Dar es Salaam kutajwa kuwa na watu wengi lakini bado makazi yake yako kiholela.

''Leo hii ukitaka kuona ladha ya Dar es salaam, uwe unashuka na ndege halafu rubani afanye makusudi asikupitishe maeneo ya Mbezi, akupitishe maeneo ya Majohe, Vingunguti,  Mji uko hovyo, umejengwa kiholela, hatujafanya uchunguzi wa kuona namna ya miji yetu ilivyo holela na majanga mangapi tumeshindwa kuwaokoa wananchi wetu kwa kukosa mipango miji mizuri ya namna miji yetu ilivyojengwa'' amesema Waziri Jafo.