
Akihutubia maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Nguzo Nane wilayani Maswa, mkoani Simiyu siku ya Jumapili Februari 16, 2025, Majaliwa amesema kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, CCM itaendelea kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana, ili wagombea wa chama wasiwe na kazi kubwa ya kueleza waliyoyafanya, bali waombe kura tu.
"CCM ni chama kikubwa, chama pendwa na chama kinachoaminiwa. Kina sera zinazotekelezeka, kikiahidi, kinatekeleza. Wanamaswa, leo mpo hapa na Mheshimiwa Nyongo (Mbunge wa Maswa Mashariki), anawapasha yanayotekelezwa ili mgombea wetu atakapofika hapa, kazi yake iwe ni ndogo ya kuomba kura," amesema Majaliwa.
Majaliwa amebainisha kuwa wakati wa kampeni, Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, watafika Maswa kuzungumza na wananchi na kueleza mipango yao kwa miaka mitano ijayo.
"Wakati wa kampeni, Mheshimiwa Rais Samia na mgombea mwenza wake Dkt. Nchimbi watakuja Maswa kuomba ridhaa yenu. Tunataka kazi yao iwe nyepesi kwa sababu tayari mmeona kazi nzuri iliyotekelezwa," amesema.
Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Hussein Mwinyi, ambaye ni Mgombea Urais kwa upande wa Zanzibar, ataendelea na kampeni zake visiwani humo huku chama kikiendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha maendeleo yanafika kila kona ya nchi.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa chama kinachoweka mbele utulivu wa nchi, mshikamano wa Watanzania, na usimamizi wa huduma muhimu kwa wananchi hata katika maeneo ya vijijini.
"CCM bado ipo imara katika kuwahudumia wananchi, kuhakikisha nchi yetu inakuwa na utulivu, mshikamano, na maendeleo. Mahitaji muhimu ya wananchi yataendelea kufikishwa hadi ngazi ya vijiji na vitongoji kwa usimamizi wa viongozi wa chama na serikali," amesisitiza.
Kwa upande wake Mbunge wa Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Haroon Nyongo amesema Jimbo la Maswa limepata fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema katika sekta ya afya, kumetekelezwa ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba na ujenzi wa hospitali akitolea mfano Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambayo ilipata zaidi ya Shilingi milioni 300 iliyofanikisha ujenzi wa jengo la kupokea wagonjwa wa dharura na kununua vifaa, akilitaja jengo hilo kuwa matunda ya Rais Samia Suluhu Hassan.