Jumamosi , 26th Oct , 2024

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana, Dkt.Bryson Kiwelu, anaomba wananchi na wadau wa Afya nchini kuwaunga mkono kufanikisha kampeni ya kuchangia maboresho na upanuzi wa jengo la mama na mtoto ili kupanua wigo wa huduma za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Dkt.Bryson Kiwelu, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Amana

Dkt.Kiwelu anasema Hospitali hiyo inapokea rufaa kutoka vituo zaidi ya 200 kwa wilaya ya Ilala hivyo mahitaji ni makubwa ukilinganisha na miundombinu iliyopo.

Aidha anasema wanataka kufanya upanuzi wa majengo, kuongeza ghorofa moja,  ukarabati wa mifumo ya maji taka, kisima cha Maji kitakachoweza kuhifadhi maji lita 4 kwa sababu kisima kilichopo sasa hakitoshelezi kutokana na huduma za usafishaji damu zinazofanyika kwenye Hospitali hiyo pamoja na vitanda 25 .

Jumla ya gharama za upanuzi huo ni shilingi bilioni 3.2 na mpaka sasa kupitia harambee iliyofanywa na Hospitali hiyo kwenye chakula cha usiku cha marafiki wa Amana kiliyofanyika Oktoba 25, 2024 imepatikana Shilingi bilioni 1.2 kwahiyo bado inahitajika shilingi bilioni 2 ili kuweza kufanikisha upanuzi huo.