
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Ameyasema hayo Ijumaa ya Januari 4, 2019 wakati akizungumza na wadau wa kahawa wa mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Jimbo, wilayani Mbinga mkoani humo.
Amesema kuanzia sasa kahawa yote itakayozalishwa nchini ni lazima iongezewe thamani na hakuna kahawa yenye maganda itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.
“Hairuhusiwi kutoa kahawa nchini na kuiuza nje ya nchi ikiwa bado na maganda, ni lazima iongezewe thamani ndipo ipelekwe katika masoko ya nje ya nchi ili iuzwe kwa bei nzuri. Hatua hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na kusaidia kulinda uwekezaji wa viwanda uliofanyika nchini", amesema Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu pia ameziagiza halmashauri zinazolima kahawa nchini kuwa na kitalu chenye miche zaidi ya laki mbili ifikapo mwisho wa mwezi wa pili mwaka huu.
“Wakati utakapofika uongozi wa Wizara ya Kilimo utakwenda kukagua iwapo agizo hili limetekelezwa’’, ameongeza.
Akizungumzia kuhusu madeni ya wakulima, aliagiza watendaji wote wa AMCOS waliohusika watafutwe na walipe deni.
“Kwa sasa Serikali haina taratibu za kununua madeni ya chama chochote cha ushirika. Kuendelea na utaratibu huo kunachochea viongozi wa ushirika kufuja mali za ushirika. Lazima watambue ukifuja fedha za wanaushirika , Serikali iko na wewe”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema minada yote ya kahawa itafanyika kwenye maeneo yanayolima ambayo yamegawanywa kwa kanda 1.Moshi (Kilimanjaro,Arusha,Tanga,Manyara) 2. Kagera ( Kigoma, Geita, Kagera, Mara) 3. Songwe ( Rukwa,Mbeya,Iringa,Katavi), na Mkoa wa Ruvuma utafanyika wilayani Mbinga .