Jumatatu , 17th Dec , 2018

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitahadharisha kaya ambazo bado hazijarudi katika makazi yao ya awali kutokana na nyumba zao kuezuliwa na upepo na mvua kali kurejea mara moja kwenye makazi yao badala ya kuishi kwenye mikusanyiko katika majengo ya serikali.

Nyumba iliyobomoka kwa maafa ya mvua.

Amesema lengo la kuwataka wananchi hao warudi kwenye makazi yao ni kuhakikisha magonjwa ya mlipuko hayatokei, na ni vyema waathirika hao wakajibane kwa ndugu ambao nyumba zao hazikuathirka na kusisitiza kuwa kujisitiri katika majengo ya serikali ni kwa dharura tu.

"Tusingependa wandelee kukaa pale, kuna hatari nyingine ya magonjwa ya mlipuko kuwaweka watu zaidi ya 200 sehemu kama ile, miundombinu ya vyoo haitoshi, kwahiyo pale ni pa muda mfupi, jamani wale watu si wana ndugu?, hatuwezi kubanana huko?," alimalizia kwa kuuliza wakati akisisitiza jambo hilo."

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan haule alitoa taarifa fupi juu ya walichokifanya baada ya maafa kutokea na kusema kuwa maafa hayo yaliathiri vijiji vinne na kitongoji kimoja katika wilaya ya sumbawanga.

"Katika Wilaya yetu maafa haya pia yalitokea kwenye vijiji kama vinne pale (kijiji) cha Muze, kule (Kijiji cha) Msia tumepata taarifa shule ya msingi ya Msia yote imeanguka lakini pia katika kijiji cha Mpwapwa na kule Tunko na kwenye kata hii kuna vijiji viwili na kitongoji cha Kituku," Alisema