
Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania limewafukuza kazi askari wake wanne wa jeshi la polisi kutokana na makosa ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova amesema uchunguzi wa wa awali umeonyesha kuwa askari hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na tukio la tarehe 9 mwazi huu eneo la Mbezi Beach A, ambapo majambazi wapatao 15 walifika katika ofisi ya kampuni ya kichina inayojulikana kwa jina la Hong Yang na kuvamia ofisi hiyo na kupora vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha taslimu na simu na kisha kutoweka.
Askari waliofukuzwa kazi wanatoka katika vikosi mbalimbali na wametajwa kuwa ni askari wenye namba E.6396 CPL Rajabu Mkwenda kutoka Makao Makuu ya Polisi, F. 9412 EC Simon wa kituo cha polisi Kati, F. 9414 EC Albernus Koosa wa kikosi cha bendi ya polisi Dar es Salaam na F. 9512 EC Seleman wa kituo cha polisi Kigamnboni.