Jumatano , 6th Mar , 2019

Siku chache baada ya Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kutangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi, aliyekuwa mtu wake wa karibu Hamis Mgeja naye ametangaza kuhamia CCM akitokea Chama Cha Demokrasia Maendeleo CHADEMA.

Mgeja alishawahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga ambapo mnamo Julai 2015 baada ya Waziri huyo Mkuu Mstaafu kutangaza kuhamia CHADEMA, naye alitangaza kumfuata.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mgeja amesema kwa sasa ameamua kurudi chama chake cha zamani kwa kile alichokisema  kuwa mambo waliyokuwa akiyapigania, hivi sasa yanafanywa na Rais Magufuli.

"Leo Marchi 06, 2019 nimeamua rasmi kuondoka CHADEMA na sitawaunga mkono tena, ndugu zangu waliumia sana wakati najiunga na CHADEMA lakini leo nawaomba radhi na natamka rasmi nimeamua kurudi nyumbani", amesema Hamis Mgeja.

Marchi 1, 2019 Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa alitangaza uamuzi wa kurejea Chama Cha Mapinduzi baada ya kukaa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa zaidi ya miaka 3.