Alhamisi , 29th Mei , 2014

Mahakama ya wilaya ya Morogoro imempandisha kizimbani Mohamed Haji Mgembe, akikabiliwa na mashtaka  ya kumbaka na kumlawiti  mwanafunzi mwenye umri wa miaka 12.

Watuhumiwa wakiwa katika eneo la Mahakama

Mahakama ya wilaya ya Morogoro imempandisha kizimbani Mohamed Haji Mgembe, akikabiliwa na mashtaka  ya kumbaka na kumlawiti  mwanafunzi wa darasa la Tano katika shule ya msingi msamvu ndege wengi katika manispaa ya morogoro, mwenye umri wa miaka 12.

Mshtakiwa huyo Mohamed Haji Mgembe(59) mkazi wa mtaa wa ndege wengi manispaa ya Morogoro, amefikishwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Regina Futakamba, na kusomewa mashtaka mawili yanayomkabili  na  mwendesha mashtaka mwandamizi wa serikali Sunday  Hyera, aliyedai,kwamba kati ya  Mei  mwaka 2013 hadi Mei mwaka huu, mshtakiwa kwa nyakati tofauti, alikuwa akimwingilia kwa njia ya kawaida na kinyume na maumbile mwanafunzi huyo, kitendo kilichompunguzia jitihada za masomo na kumfanya kutembea kwa tabu, hadi  walimu walipomhoji na akamtaja mshtakiwa.

Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na polisi waliweka mtego na kumtia mbaroni mshtakiwa akiwa na mwanafunzi huyo nyumbani.
 
Mshtakiwa amekana mashtaka hayo yanayomkabili na kurudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ikiwemo kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, na mmoja awe mtumishi wa serikali, kampuni au shirika lililosajiliwa kisheria, ambao kila mmoja ataweka dhamana ya kimaandishi ya shilingi milioni moja, ambapo shauri hilo limepangwa kufikishwa tena mahakamani hapo Juni 12, majira ya saa Nne Asubuhi.
 
Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto ikiwemo kubakwa na kulawitiwa, watu waliofika mahakamani hapo wameomba sheria kuchukua mkondo wake ili kukomesha vitendo vya aina hiyo kwenye jamii, na hata kutoa taarifa ya matukio hayo na kuwaelimisha watoto wao umuhimu wa kujitambua na kujieleza.