Alhamisi , 7th Mar , 2019

Mama mzazi wa Marehemu Ruge Mutahaba, Dkt. Christiana Mutahaba amesema kuwa kifo cha mtoto wake kimemuonesha kuwa ule muda aliokuwa mbali na familia aliutumia kuwatumikia watanzania.

Ndugu wa karibu na familia ya Profesa Mutahaba, wakiwafariji familia baada ya kuondokewa na kijana wao Ruge Mutahaba.

Mama Mutahaba amesema kuwa amekuwa akigombana na mwanaye kipindi cha uhai wake kutokana na muda mwingi kuutumia katika kazi na muda mchache sana kutumia na familia.

"Mwanangu naomba huko aliko anisamehe sana kwani nimeliona hili baada ya kifo chake, Ruge nilikuwa namsema sana mambo yake yakuwa bize kiasi kwamba nyumbani kuna muda hatumuoni muda mrefu, lakini kumbe alikuwa akiwatumikia watanzania", amesema  Dkt. Christiana Mutahaba.

Katika hatua nyingine amesema kuwa atafurahi kuona mambo yaliyoanzishwa na mwanaye yakitekelezwa na kuendelezwa kwa lengo la kuenzi aliyopenda kuifanyia jamii.

Aidha amevitaka vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kile alichodai kuwa mara kadhaa mwanaye alikuwa akizushiwa amefariki jambo lililokuwa likiiumiza familia.

Marehemu Ruge Mutahaba alifariki dunia Februari 26 akiwa nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu, na amezikwa nyumbani kwao Kiziru wilayani Bukoba mkoani Kagera Machi 4, 2019